JUMANNE, JUMA LA 16 LA MWAKA WA KANISA
SOMO 1
Mik. 7:14 – 15, 18 – 20
Walishe watu wako kwa fimbo yako, kundi la urithi wako,
wakaao peke yao, mwituni katikati ya Karmeli; na walishe katika Bashani na
Gileadi, kama siku za kale. Kama katika siku zile za kutoka kwako katika nchi
ya Misri nitamwonyesha mambo ya ajabu.
Ni nani aliye Mungu kama wewe, mwenye kusamehe uovu, na
kuliachilia kosa la watu wa urithi wake waliosalia? Hashiki hasira yake milele,
kwa maana yeye hufurahia rehema. Atarejea na kutuhurumia; atayakanyaga maovu
yetu; nawe utazitupa dhambi zao zote katika vilindi vya bahari. Wewe
utamtimilizia Yakobo kweli yako, na Ibrahimu rehema zako, ulizowaapia baba zetu
tangu siku za kale.
Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 85:1 – 7 (K) 7
(K) Ee Bwana, utuonyeshe rehema zako.
Bwana, umeiridhia nchi yako,
Umewarejeza mateka wa Yakobo.
Umeusamehe uovu wa watu wako,
Umezisitiri hatia zao zote.
Umeiondoa ghadhabu yako yote,
Umerudi na kuuacha ukali wa hasira yako. (K)
Mungu wa wokovu wetu, uturudishe,
Uikomeshe hasira uliyo nayo juu yetu.
Je! Utatufanyia hasira hata milele?
Utadumisha ghadhabu kizazi hata kizazi. (K)
Je! Hutaki kurudi na kutuhuisha,
Watu wako wakufurahie?
Ee Bwana, utuonyeshe rehema zako,
Utupe wokovu wako. (K)
SHANGILIO
2 Kor. 5:19
Aleluya, aleluya,
Mungu alikuwa ndani ya Kristu, akiupatanisha ulimwengu na
nafsi yake. Ametia ndani yetu neno la upatanisho.
Aleluya.
INJILI
Mt. 12:46 – 50
Yesu alipokuwa katika kusema na makutano, tazama, mama
yake na ndugu zake walikuwa wakisimama nje wataka kusema naye. Mtu mmoja
akamwambia, Tazama, mama yako na ndugu zako wamesimama nje, wanataka kusema
nawe. Akajibu, akamwambia yule aliyempasha habari, Mama yangu ni nani? Na ndugu
zangu ni akina nani? Akawanyoshea mkono wanafunzi wake, akasema, Tazama, Mama
yangu na ndugu zangu! Kwa maana yeyote atakayeyafanya mapenzi ya Baba yangu
aliye mbinguni, huyu ndiye ndugu yangu, na umbu langu, na mama yangu.
Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo.
0 comments:
Post a Comment