Kongamano la Kitaifa la Vijana Njombe liendelee kuwa chachu ya imani nchini

DSC_0531

KONGAMANO la Kitaifa la vijana Wakatoliki Tanzania kutoka majimbo 32 lilianza Juni 09 – 15/ 2015 imekuwa chachu ya imani ya Kanisa Katoliki baada ya vijana kulishwa ujumbe wa imanikutokana na mada mbalimbali zilizotolewa na viongozi mbalimbali wa imani ya Kanisa Katoliki. 
Kulingana na mafundisho waliyopata hususani Askofu Gervasi Nyaisonga aliyewapa hamasa ya imani vijana kuwa wavumilivu wa changamoto wanazozipata kwani nyingine hazikwepeki. Changamoto hizo zinahitaji uvumilivu wa imani ambao utawafanya wakabidhi mizigo hiyo kwa Kristo.
Tunaamini kuwa vijana wetu wana mizigo mingi, ikiwa ni mizigo ambayo haikwepeki, mizigo ya kujitakia, mizigo ya kusakiziwa na mizigo ya kurubuniwa. Kwa mantiki hiyo mimi kama mratibu wa vijana taifa niliona nivizuri wanakongamano wakaongozwa na dhamira hii “Njoni kwangu nyinyi nyote msumbukao na kuelemewa na mizigo, nami nitawapumuzisha …Maana, nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi” (Mt. 11: 28, 30).
Ninaamini kwamba pamoja na mizigo hiyo, kitulizo chao ni Kristo ambaye anawapatia matumaini na furaha ya kweli. Pia, wanakongamano hao walipata fursa ya kuzindua maadhimisho ya miaka 150 ya uinjilishaji Tanzania ambapo kilele chake ni 2018. Kumbe basi uzinduzi huo uliongozwa na kauli mbiu isemayo “Furaha ya injili kwa vijana, Jubilei ya miaka 150 ya uinjlishaji Tanzania.
Chachu ya imani iliyojionyeha kwenye Kongamano hilo ilitokana na mada ambazo zilitolewa. Mada zilizotolewa zilimgusa kila kijana, na vijana wote kwa pamoja waliahidi kuzifanyia kazi na hasa kuziweka katika maisha na matendo yao ya kila siku. Mada hizo ni: Miaka 150 ya uinjilishaji Tanzana na Uinjilishaji mpya iliyotolewa na Katibu Mkuu Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Padri Raymond Saba ambaye alitoa hamasa juu ya imani yetu Katoliki.
Nikimnukuu alieleza; “Kizazi cha sasa kina changamoto tofauti na zile za enzi za wamisionari wa kwanza. Tatizo lipo kwenye namna ya kuinjilisha. Tuna mitandao ya kijamii ambayo ikitumika ipasavyo tutainjilisha kwa nyakati zetu hizi za utandawazi.
Tatizo jingine ni ujinga wa imani kwamba wakatoliki hatuijui vizuri imani yetu. Hatusomi maandiko na vitabu vya dini, hatuijui Katekesimu yetu ndio maana tukipewa changamoto kidogo tunahama makanisa. Makleri hatufundishi, waamini hawafundishiki. Tutafundisha nini kamahatusomi na hatujui imani yetu, mtaitetea imani yenu kivipi kama hamtaki kufundishwa na hamsomi maandiko?” mwisho wa kunukuu.
Hii imeleta hamasa pale vijana walipoona wametoka gizani na kuona mwanga wa wajibu walionao wa kufuatilia mafundisho ya Kanisa.
Mada nyingine ilikuwa ni ‘Kijana na utandawazi’ iliyotolewa na Padri Titus Amigu wa Jimbo Katoliki Lindi ambaye aliwapa vijana changamoto ya kuwa makini na udanganyifu wa utandawazi wakiwemo waganga wa kienyeji wanaotumia njia za mkato kutoa suluhisho za matatizo yao. Vijana walionekana kuguswa na mada hiyo hata kutaka mada hizo kutolewa kwenye vyomba vya habari hususani gazeti kiongozi ili wasome kwa kina zaidi ili kupambana na Changamoto za vijana kwa wakati huu.
Mada nyingine zilikuwa Ujasiriamali, Kijana na maisha ya familia, Kijana na afya yake na Biblia na Sakramenti. Baada ya mada hizo vijana wameonekana kushiba mambo ambayo walikuwa hawayafahamu.
Kijana Mercy Joseph kutoka Jimbo Katoliki Morogoro ameeleza kuwa, amefurahishwa na mada zilizotolewa hususani zilizogusa imani ya Kanisa Katoliki.
“Mimi naona tumejengwa upya kiimani kutokana na mada zilizotolewa. Kongamano hili ni chachu ya kuamsha ari ya kuifahamu zaidi imani yetu na kuiishi kwa kuitetea kinadharia bila kuyumbishwa. Ninawasihi vijana wenzangu kushika mafundisho tuliyopewa na kama tutayaishi kweli, tuna kila sababu ya kusherehekea miaka 150 ya ukristo wetu,” ameeleza Mercy.
Chachu hiyo ya imani ilionekana si kwa wanakongamano tu, bali hata kwa Taifa nzima la Mungu Jimboni Njombe, kwa njia ya maandamano ya vijana yaliyofanyika siku ya Jumapili tarehe 14/06/2015. Maandamano hayo yalianzia kwenye shule ya Mtakatifu  Josephine hadi kwenye Kanisa lenye kiti cha Kiaskofu Jimboni Njombe ambapo maadhimisho ya misa ya kufunga Kongamano hilo yalifanyikia. Askofu Mkuu Damiani Dallu, katika mahubiri yake wakati wa misa ya kufunga Kongamano hilo iliyoongowa na Askofu Alfred Maluma, Askofu wa Jimbo la Njombe na mwenyeji wa Kongamano, alisisitiza mambo makuu sita
(a) Furaha ya Injili na upendo wa Kristo uwaongoze vijana katika maisha yao ya kila siku.
(b) Vijana wailinde Imani yao kwa kuishi maisha ya uadilifu
(c) Vijana wajivunie utaifa wao na kuipeperusha bendera ya Taifa kila mahali
(d) Vijana wayatunze mazingira
(e) Vijana wasirubuniwe
(f) Wajiandikishe kwenye daftari la kudumu la wapiga kura,wajitokeze katika nafasi mbalimbali za uongozi, na kushiriki katika uchaguzi wa madiwani, Wabunge na raisi hapo Okitoba mwaka huu.
Ninaomba chachu hiyo ya Imani isambae kwa kila kijana wa Kanisa Katoliki Tanzania, ili makuu ya Mungu yajidhihirishe kwa kila kijana na kwa pamoja waweze kuyatakatifuza malimwengu. Ninawaomba maaskofu wetu na Walezi wote wa vijana katika majimbo yetu Katoliki wawe mstari wa mbele katika kazi hiyo kubwa ya kukuza na kuendeleza hiyo chachu ya Imani kwa vijana.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment