Mama
Theresa wa Calcutta anatarajiwa kutangazwa kuwa Mtakatifu hapo Tarehe 4
Septemba 2016, kielelezo na shuhuda wa huruma ya upendo wa Mungu
unaomwilishwa kwa wagonjwa, maskini na wote wanaosukumwa pembezoni mwa
jamii kwani upendo kwa jirani ndicho kipimo ambacho Yesu atakitumia siku
ya mwisho kuwahukumu wazima na wafu! Maskini ni kundi lisilopendwa na
wengi, kumbe hili ndilo kundi ambalo Mama Theresa wa Calcutta anawaalika
waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuonesha upendo wao
kwao.
Huu ni muhtasari wa kitabu ambacho kimeandikwa kwa heshima ya Mama
Theresa wa Calcutta na Baba Mtakatifu Francisko kukiandikia dibaji yake!
Baba Mtakatifu anawataka vijana wanaoshiriki maadhimisho ya Siku ya
Vijana Duniani kuwa ni vyombo na mashuhuda wa ujenzi wa madaraja ya
kuwakutanisha watu kwa kufutilia mbali mantiki ya utengano na ubaguzi
unaoendelea kupaliliwa na wengi duniani. Vijana wawe na ujasiri wa
kuachana na tabia ya woga usiokuwa na mvuto wala mashiko na badala yake
wawe ni mashuhuda na vyombo vya huruma na mapendo kwa maskini na
wahitaji zaidi.
Mama Theresa wa Calcutta anakaza kusema, Ukoma na Kifua kikuu ni
magonjwa ambayo hayawezi kufua dafu kwa upweke hasi unaoweza kumfanya
mwanadamu kuchungulia na hata wakati mwingine kuonja kaburi! Upweke ni
chanzo cha mipasuko ya kijamii, ukosefu wa amani, vita na majanga
yanayomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo. Baba Mtakatifu
Francisko katika dibaji ya kitabu hiki anakazia mambo mafuatayo: Sala,
upendo, huruma, familia na vijana. Anakumbusha kwamba, Kanisa katika
maisha na utume wake linaendeleza kazi ya ukombozi iliyoanzishwa na
Kristo Yesu na kwamba, kuna maskini wanaohitaji kuonjesha huruma na
upendo wa Mungu katika maisha yao.
Mama Theresa wa Calcutta anawahamasisha waamini kujichotea nguvu ya
huruma na upendo katika kisima cha: Sala, Ibada ya Kuabudu Ekaristi
Takatifu na maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, ili kuweza
kumwilisha sala katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Sala
iwawezeshe waamini kukutana na kuzungumzana na Kristo Yesu; kuomba
rehema na neema ili kuwa kweli ni watu wanaoweza kuthubutu kujisadaka
kwa ajili ya Mungu na jirani zao; kwa kuwaangalia wote kwa jicho la
upendo linalopyaisha maisha ya watu!
Baba Mtakatifu anasema, upendo ni fadhila inayomwezesha mwamini kuwa
kweli ni Msamaria mwema kwa jirani yake anayeogelea katika shida na
magumu ya maisha: kiroho na kimwili. Upendo uwawezeshe waamini kuwa ni
mashuhuda wa huruma inayoganga na kuponya madonda na majeraha ya maisha
ya mwanadamu; ni ushuhuda wa faraja ya Mungu kwa madonda ya binadamu!
Yote haya yanawezekana ikiwa kwama mwaminifu amefungamanisha maisha yake
na Kristo Yesu, tayari kushuhudia uwepo na ukaribu wa Mungu mwingi wa
huruma kwa waja wake!
Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi
mema kutafakari kwa makini huruma ya Mungu na kuimwilisha katika matendo
ya huruma: kiroho na kimwili tayari kupambana na umaskini, ujinga na
maradhi mambo yanayodhalilisha utu na heshima ya binadamu. Maskini ni
kundi ambalo linaonjeshwa kwa namna ya pekee huruma ya Mungu, kumbe,
waamini wawe kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu kwa maskini
na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.
Mama Theresa wa Calcutta aliyaandika matendo ya huruma: kiroho na
kimwili katika maisha na utume wake, yakawa ni chachu ya utakatifu wa
maisha, kumbe, ni jambo linalowezekana hata kwa waamini wengine kuiga
mfano huu bora! Mama Theresa alionesha karama na utajiri wa kimama,
akawapokea na kuwahudumia watu wote pasi na ubaguzi. Alikuwa na jicho la
pekee hasa kwa vijana waliokuwa wanaishi katika mazingira magumu na
hatarishi baada ya familia zao kusambaratika kutokana na sababu mbali
mbali.
Bikira Maria ni mfano wa Umama unaoguswa na mahangaiko ya wengine,
tayari kuyajibu kwa njia ya huduma makini! Waamini pamoja na watu wote
wenye mapenzi mema wanahamasishwa kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya
faraja ya Mungu kwa familia zao kwa njia ya sala. Familia inahitaji
kusimikwa katika upendo, umoja na kufanya kazi kwa juhudi, bidii na
maarifa! Kwa kutekeleza yote haya, familia zinakuwa ni zawadi kubwa
inayoweza kutolewa kwa Kanisa!
Mama Theresa wa Calcutta anawataka vijana kwa namna ya pekee kujenga
maisha na uwepo wao kwa kumzunguka Kristo Yesu, ufunuo wa Huruma ya
Mungu; mwamba thabiti na mwaminifu katika ahadi zake hata kama mwanadamu
atakengeuka na kuasi. Baba Mtakatifu anawataka vijana wa kizazi kipya
kukita maisha yao katika matumaini na kamwe wasithubutu kutoa nafasi kwa
wajanja wachache kupoka matumaini yao, bali waendelee kushikamana na
kumpenda Mungu; huku wakijenga madaraja yanayowaunganisha watu, kwa
kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa maskini na wahitaji
zaidi.
Baba Mtakatifu Francisko anawataka Vijana wawe na ujasiri wa
kupambana na changamoto za maisha, daima wakiwa na malengo ya juu pamoja
na kuwashirikisha vijana wenzao fursa na mafanikio ya maisha. Vijana wa
kizazi kipya warutubishe maisha yao kwa njia ya Neno la Mungu,
Sakramenti na Sala ili kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya
Mungu katika medani mbali mbali za maisha. Mwishoni, Baba Mtakatifu
anawatakia watu wote amani na furaha ya huruma ya Mungu iweze kutawala
duniani kwa maombezi ya Mama Theresa wa Calcutta!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
0 comments:
Post a Comment