Baba Mtakatifu Francisko amemteua Mheshimiwa Padre Flavian Matinde Kassala kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki Geita, Tanzania.

Kabla ya uteuzi huu, Askofu mteule Kassala alikuwa ni mkurugenzi wa Kitivo cha Stella Maris, Mtwara, Chuo kikuu cha Mtakatifu Agostino cha Tanzania.

Mheshimiwa Padre Flavian Matinde Kassala

Askofu mteule Kassala alizaliwa tarehe 4 Desemba 1967, Parokia ya Sumve, Jimbo kuu la Mwanza. Alipata masomo yake ya Sekondari kutoka Seminari Ndogo ya Mtakatifu Pio wa X, iliyoko Makoko, Jimbo Katoliki la Musoma.

Alijiendeleza zaidi kwenye Seminari Ndogo ya Sanu Jimbo Katoliki Mbulu. Akapata majiundo ya falsafa kutoka Seminari ya Mtakatifu Anthony wa Padua, Maarufu kama Ntungamo, iliyoko Jimbo Katoliki la Bukoba.

Askofu mteule Kassala alijipatia majiundo yake ya kitaalimungu kwenye Seminari kuu ya Mtakatifu Paulo, maarufu kama Kipalapala iliyoko Jimbo kuu la Tabora.

Baada ya safari hii ndefu katika maisha na wito wa kipadre, akapewa Daraja Takatifu la Upadre hapo tarehe 11 Julai 1999 kama Padre wa Jimbo Katoliki Geita.

Baada ya Upadrisho kati ya mwaka 1999 hadi mwaka 2002 alikuwa ni Paroko usu, Parokia ya Sengerema, Jimbo Katoliki la Geita. Mwaka 2002- 2004 alikuwa ni mlezi na Padre wa maisha ya kiroho Seminari ndogo ya Bikira Maria Malkia wa Mitume, Jimbo Katoliki Geita pamoja na kuwa ni Mkurugenzi wa Jimbo Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa.

Askofu mteule Flavian Kassala kuanzia mwaka 2004 hadi mwaka 2012 alitumwa na Jimbo kujiendeleza zaidi katika utume wa vijana na katekesi katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Wasalesiani, kilichoko mjini Roma na hapo akajipatia shahada ya nguvu ya uzamivu.

Akiwa mjini Roma kwa miaka kadhaa alishiriki kuandaa makala ya vijana Radio Vatican, makala zilizokuwa zinagusa maisha na changamoto za vijana wa kizazi kipya.

Kunako mwaka 2013 Askofu mteule Kassala akarejea Jimboni Geita na huko akapewa dhamana ya kuratibu miradi ya Jimbo.

Kuanzia mwaka 2013- 2015 akepewa dhamana ya kusimamia na kufundisha Chuo Kikuu cha SAUT, Kitivo cha Utalii, Arusha. Kunako mwaka 2015, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania likamhamishia Kitivo cha Stella Maris, Mtwara kama mkurugenzi.

Itakumbuka kwamba, Jimbo Katoliki Geita limekuwa wazi kuanzia tarehe 14 Machi 2014, baada ya Baba Mtakatifu Francisko kumhamisha na kumpandisha hadhi Askofu Damian Dallu kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Songea

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Cc:
Padre Richard A. MjigwaChuo kikuu cha SAUT

Askofu mkuu Damian DalluJimbo Katoliki Geita, Tanzania

Askofu Flavian M. Kassala 28/04/2016

Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment