Tunapojiandaa na Mwezi wa Maria ambapo tunasali Rozari Takatifu pamoja naye, Mwandishi anaeleza uhusiano wa Mungu na mwanadamu kupitia Bikira Maria kupitia Agano la Kale ambalo ni matayarisho ya Agano Jipya. Agano Jipya lilianza rasmi kwa maneno ya Bikira Maria alipojiweka mikononi mwa Mungu kwa niaba ya taifa jipya la Mungu, yaani Kanisa: “Tazama, mimi ni mtumishi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema.” Soma kwa makini.
AGANO la Kale lilikuwa ni matayarisho ya Agano Jipya ndiyo maana Yesu anasema kuwa amekuja ili kulikamilisha.
Kuna sababu kuu mbili ambazo zinalifanya Agano la Kale liwe ni matayarisho na lisiwe limekamilika: Agano la Kale lilifanywa kati ya Mungu na taifa moja tu la Israeli kwa njia ya nabii Musa.
Agano la Kale halikuwa na nguvu ya kuiondoa dhambi ya asili iliyoletwa kwa njia ya shetani, Adamu na Eva. Kwa njia ya Yesu Kristo, agano linakuwa sio tena kati ya Mungu na Israeli, bali Agano Jipya kati ya Mungu na watu wote.
Ni agano lenye nguvu ya kuiondoa dhambi ya asili na dhambi binafsi. Kwa hiyo ni Agano Jipya na la milele: Nao walipokuwa wakila, Yesu alitwaa mkate, akabariki, akaumega, akawapa wanafunzi wake, akasema, “Twaeni, mle; huu ndio mwili wangu.”
Akakitwaa kikombe, akashukuru, akawapa, akisema, “Nyweni nyote katika hiki; kwa maana hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi.”Mathayo 26:26-28 Agano hilo jipya na la milele lililoletwa na Yesu lilitabiriwa na manabii tangu zamani kuwa litakuwa ni agano si la Waisraeli peke yao bali ni la mataifa yote duniani.
Nabii Isaya alilitangaza kuwa litakuwa ni agano litakaloleta ukombozi kwa mataifa yote duniani yatakayomtambua Mungu wa kweli: Hubirini, toeni habari, naam, na wafanye mashauri pamoja!
Ni nani aliyeonesha haya tangu zamani za kale? Ni nani aliyehubiri hapo zamani? Si mimi, Bwana? Wala hapana mwingine zaidi ya mimi. Niangalieni mimi, mkaokolewe, enyi ncha zote za dunia, maana mimi ni Mungu, hapana mwingine. Isaya 45:21-22 Nabii Yeremia pia alitabiri habari za Agano Jipya miaka mingi kabla ya Yesu kuja duniani.
Nabii Yeremia alilitangaza agano hilo kuwa litahusu msamaha wa dhambi binafsi. Dhambi binafsi ni tofauti na ile dhambi ya Asili. Dhambi ya Asili ni ile tuliyoirithi toka kwa mama yetu Eva.
Dhambi binafsi ni yetu wenyewe tunapovunja amri za Mungu (agano la Sinai) kwa makusudi. Nabii Yeremia pia analitofautisha Agano la Kale na Agano Jipya kwani katika Agano la Kale amri za Mungu ziliandikwa katika mawe mawili, kumbe katika Agano Jipya amri za Mungu zinaandikwa ndani ya mioyo ya watu: Angalieni, siku zinakuja, asema Bwana, nitakapofanya agano jipya na nyumba ya Israeli, na nyumba ya Yuda.
Si kwa mfano wa agano lile nililolifanya na baba zao, katika siku ile nilipowashika mkono, ili kuwatoa katika nchi ya Misri; ambalo agano hilo walilivunja, ingawa nalikuwa mume kwao, asema Bwana.
Basi agano hili ndilo nitakalofanya na nyumba ya Israeli, baada ya siku zile, asema Bwana: nitatia sheria yangu ndani yao, na katika mioyo yao nitaiandika. Nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu. …..Asema Bwana; “maana nitausamehe uovu wao, wala dhambi yao sitaikumbuka tena”. Yeremia 31:31-33 Nabii Ezekieli naye alilitangaza Agano Jipya kuwa litakuwa ni la milele na hasa litafanywa ili kurudisha amani kati ya Mungu na mataifa yote ya dunia.
Kwa njia ya agano hilo jipya, Mungu ataweka makao yake kati ya watu wote na wote watamtambua kuwa ni Mungu wao: “Tena nitafanya agano la amani pamoja nao, litakuwa agano la milele pamoja nao.
Nami nitawaweka na kuwazidisha, na patakatifu pangu nitapaweka katikati yao milele. Tena maskani yangu itakuwa pamoja nao; nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.
Na mataifa watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, mimi niwatakasaye Israeli, patakatifu pangu patakapokuwa katikati yao milele.” Ezekieli 37:26-28 Hivyo basi, neno agano katika Historia ya Ukombozi linabeba uzito mkubwa katika kueleza uhusiano wa Mungu na wanadamu.
Hii ndiyo sababu Biblia inagawika katika sehemu kuu mbili: Agano la kale na Agano Jipya. Katika Historia ya Ukombozi, maneno kale na jipya yanatofautishwa katika namna na wakati agano lilivyofanywa. Neno kale hapa halina maana ya kitu cha zamani kilichopoteza thamani bali lina maana ya kitu kilichofanyika awali na chenye thamani hata leo. Ukale wake upo katika wakati au kipindi, yaani awali, kabla ya Yesu.
Ukale huo pia upo katika namna au mtindo, yaani Mungu alifanya agano kwa njia ya watu wanaoitwa manabii. Neno jipya halina maana ya kitu kipya chenye thamani zaidi ya kile cha awali bali upya wake upo katika wakati au kipindi na namna au mtindo. Katika Agano Jipya Mungu hatumii tena manabii bali anafanya agano na watu wake wote yeye mwenyewe kwa njia ya mwanae Yesu Kristo:
Mungu ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika Mwana, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu.
Yeye kwa kuwa ni mng’ao wa utukufu wake na chapa ya nafsi yake, akavichukua vyote kwa amri ya uweza wake, akiisha kufanya utakaso wa dhambi, aliketi mkono wa kuume wa ukuu huko juu; amefanyika bora kupita malaika, kwa kadiri jina alilolirithi lilivyo tukufu kuliko lao. Waebrania 1:1-4 Agano la Kale na Agano Jipya ni sehemu mbili za Biblia zenye thamani sawa kabisa na ni sehemu mbili zinazotegemezana na kukamilishana kabisa.
Haiwezekani kulielewa Agano la kale bila Agano Jipya, pia haiwezekani kulielewa Agano Jipya bila ya Agano la Kale. Maagano yote mawili yalianza rasmi kwa maneno yanayofanana katika maudhui yake: Agano la Kale lilianza rasmi kwa maneno ya wana wa Israeli walipomwambia Mungu kwa njia ya Musa: “Hayo yote aliyoyasema Bwana tutayatenda.”
Agano Jipya lilianza rasmi kwa maneno ya Bikira Maria alipojiweka mikononi mwa Mungu kwa niaba ya taifa jipya la Mungu, yaani Kanisa: “Tazama, mimi ni mtumishi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema.”
Mwandishi ni Padri wa Jimbo Katoliki Iringa
0 comments:
Post a Comment