Kikosi cha ulinzi cha Papa kula kiapo cha utii, tarehe 6 Mei 2016

Kikosi cha ulinzi cha Papa maarufu kama Swissguards kimejizatiti kikamilifu katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. - OSS_ROM
Wanajeshi wapya wa Kikosi cha ulinzi wa Papa kutoka Uswiss, maarufu kama “Swissguards”, Ijumaa tarehe 6 Mei 2016 watakula kiapo cha utii kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, tukio ambalo linapata umuhimu wa pekee kabisa wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Jubilei ya huruma ya Mungu. Askari wa Uswiss, daima wamekuwa mstari wa mbele katika maadhimisho ya matukio mbali mbali mjini Vatican.
Padre Thomas Widermer, Padre mshauri wa kiroho wa Kikosi cha Ulinzi wa Papa kutoka Uswiss anasema, wanajeshi hawa ambao wengi wao ni vijana, wenye matumaini makubwa mbele yao, wanaunda Parokia ya pekee na kumbe, kazi ya Padre mshauri ni kuhakikisha kwamba, anawasaidia katika majiundo na ukomavu wa maisha ya kiroho na kimwili. Wanatambua kwamba, hapa Roma ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa la Kiulimwengu, kumbe hata wao wanapaswa kuwa na mtazamo na mwelekeo kama huu wanapotekeleza dhamana na utume wao kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Padre Widermer katika mahojiano maalum na Gazeti la L’Osservatore Romano anasema, kuna sababu mbali mbali ambazo zinaweza kuwasukuma vijana kutaka kujiunga na Kikosi cha Ulinzi wa Papa. Moja vijana wanataka kupata uzoefu, mang’amuzi na weledi kuhusiana na wito pamoja na taaluma ya kijeshi. Wengi wao, hii ni ni nafasi ya kukua na kukomaa katika imani, matumaini na mapendo, kwa kufanya utume wao karibu sana na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Wanatambua kwamba, ufahamu wa mazingira ya mji wa Vatican na lugha ya Kiitalia ni utajiri mkubwa ambao unaacha chapa ya kudumu katika akili na nyoyo zao wakati wote!
Padre mwongozi wa maisha ya kiroho amepewa dhamana ya kuhakikisha kwamba, anawasaidia vijana hawa wanaojiandaa kwa utume maalum, kukua na kukomaa katika maisha ya kiroho na kiutu. Kwa mfano, wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, wamejifunza kwa umakini mkubwa kuhusu dhana ya huruma ya Mungu kama inavyofafanuliwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume, Uso wa huruma, “Misericordiae vultus”.
Katika majiundo yao, wanapata katekesi ya kina na endelevu kuhusu: uaminifu, maana ya sadaka na zawadi ya maisha; ulinzi na usalama; dhamana na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro katika Kanisa la Kristo. Hiki pia ni kipindi kinachowawezesha askari hawa kupata utajiri wa kitamaduni kwa kufanya hija katika maeneo muhimu ya kihistoria. Wanajeshi hawa wanajifunza kwa kina na mapana matendo ya huruma kiroho na kimwili, kwani ni sehemu ya vinasaba vya utume wao. Mara nyingi hawa ndio wanaomsindikiza mtunza sadaka mkuu wa Papa katika kuwasaidia maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii katika mitaa ya Roma nyakati za usiku, ili kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment