Makundi ya vijana yako njiani kuelekea Poland!


Vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia wameanza kuelekea nchini Poland ili kushiriki kikamilifu maadhimisho ya Siku ya XXXI ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016.
Kardinali Ricardo Blazquez, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania anaongoza ujumbe mzito wa Maaskofu 51 wanaoongozana na vijana 30, 500 kutoka Hispania kwenda nchini Poland kuhudhuria maadhimisho ya Siku ya XXXI ya Vijana Duniani inayoongozwa na kauli mbiu “Heri wenye rehema maana hao watapata rehema”. Idara ya utume wa vijana Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania inaendelea kukamilisha mipango, ili hapo tarehe 25 Julai 2016 Siku kuu ya Mtakatifu Yakobo Mtume, wakiwa huko Czestochowa, Poland, vijana wote wanaozungumza lugha ya Kihispania waweze kushiriki katika Ibada ya Misa Takatifu itakayoongozwa na Kardinali Ricardo akisaidiana na Maaskofu Katoliki kutoka Hispania.
Baadaye, vijana hao kwa muda wa masaa mawili, watawezesha kusherehekea ujana wao huku wakiwa wameandamana na Maaskofu wao, matendo makuu ya Mungu! Waswahili wanasema, vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanataka kuwasha moto wa Injili ya huruma ya Mungu nchini Poland kwa kujenga na kudumisha imani, mapendo, umoja na udugu wa familia ya Mungu!
Taarifa zinaonesha kwamba, baada ya maandalizi ya katekesi ya kina kuhusu maadhimisho ya Siku ya XXXI ya Vijana Duniani huko Poland, vijana kutoka Uingereza wameanza kuelekea nchini Poland ili kushiriki maadhimisho ya Siku ya Vjana Duniani. Wamejiandaa kwa kukusanya fedha ya safari na kujikimu wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani. Kuna waandishi wa habari 60 ambao wanataka kuhakikisha kwamba, maadhimisho haya yanawafikia hata vijana wale ambao hawatabahatika kwenda Poland kushiriki pamoja na Baba Mtakatifu Francisko.
Hili ni tukio ambalo linapewa umuhimu wa pekee katika mitandao ya kijamii, mahali ambapo vijana wanatumia muda wao mrefu ili kupata habari, kujiburudisha na kuhabarishana yale yanayojiri katika maisha ya ujana wao! Mitandao ya kijamii ni uwanja mkubwa ambao unaweza kutumiwa na Mama Kanisa katika mchakato wa Uinjilishaji mpya miongoni mwa vijana wa kizazi kipya!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment